Thursday, February 23, 2012

BIASHARA NDOGO NDOGO NA UJASIRIAMALI

UJASIRIAMALI na BIASHARA NDOGO NGOGO
Watu wengi wamekuwa wakitumia neno Mjasiriamali kama mfanya biashara ndogondogo, kuna uhusiano baina ya ufanyaji biashara ndogo ndogo na Ujasiriamali, lakini hakuna usawa kati ya vitu hivi viwili kwa dhana zifuatazo:

Kiasi cha Fedha na Utajiri.

Mfanya biashara ndogo ndogo mara nyingi hulenga kujipatia kipato cha kujikimu kutokana na ukosefu wa kazi ya kuajiriwa au ugumu wa maisha na maisha huwa hayana matarajio makubwa sana.
Mjasiriamali hufanya biashara au shughuli yake kwa malengo na matarajio ya kujipatia kipato cha kutosha kujikimu, kufanya mambo ya maendeleo na hatimaye kuwa tajiri Mkubwa kwa kuwekea mkazo shughuli zake kwa misingi muhimu ya maendeleo.

Malengo na muda wa Mafanikio
Mfanya biashara ndogondogo anaweza maliza muda mrefu, hata maisha yake yote ikibidi kwa kujipatia kipato kidogo sana, wakati Mjasiriamali huwa na ari na kasi ya ya shughuli yake kwa kuwa na malengo na kuyaendea kwa kasi hiyo ili kupata mafanikio na kujitengenezea utajiri ndani ya muda Fulani mfano ndani ya miaka 3.

Hatari za kibiashara na kuziendea mbio nafasi.

Mjasiriamali huangalia hatari zinazoikabili biashara au shughuli yake na kuwa na tahadhari za kutosha kujiepusha na madhara yanayoweza kuepukika ili azidi kusonga mbele, pia huzitolea macho fursa zinazopita mbele yake au kwa wengine na ku improvise(kuzinadia kwa upande wake) kwa mfanya biashara ndogo ndogo wa kawaida hili halimshughulishi sana ili mradi anauza kidogo, na chakula kinapatikana basi siku zinaenda.

Uvumbuzi na Ubunifu.
Mjasiriamali hufanya Uvumbuzi na Ubunifu zaida ya mfanya biashara ndogondogo wa kawaida, uvumbuzi huu humpa changamoto zenye faida ambazo hupelekea kutajirika, Uvumbuzi huu huwa katika bidhaa au huduma husika au katika utaratibu wa kibiashara katika kufikisha kwa wateja/watumiaji wake.

Mnaonaje Ndugu zangu?, huu ni mtazamo wa kisomi wa Kijasiriamali.

Tuesday, February 21, 2012

MAANA YA UJASIRIAMALI

Nini maana ya Ujasiriamali?.

Dhana ya Ujasiriamali ina maana pana , miongoni mwa hizo ni;  Mjasiriamali ni mtu ambaye ana hamasa kubwa ya kuleta mabadiliko chanya  katika hali yake ya kiuchumi ambaye ana tabia za kipekee ili kufanikisha azma yake hiyo kwa kujishuhulisha (yaani kujiajiri) ili awe na hali nzuri zaidi kiuchumi.

Pia katika hali nyingine   Mjasiriamali  anaweza kuwa mtu yoyote ambaye anajishughulisha mwenyewe(amejiajiri) katika sekta fulani mfano: kilimo, ufugaji au biashara.

Neno Ujasiriamali lina asili ya Kifaransa " Entreprendre" sawa na Kutekeleza/Kufanya shughuli fulani mwenyewe katika uwanja wa kibiashara katika maana rahisi ni sawa na kuanzisha biashara/shughuli ya kujiajiri.

Kwa mitazamo mbalimbali ya wasomi wana muelezea  Mjasiriamali kama mtu ANAYEONGOZA, ANAYEPANGA na ALIYE NA UTAYARI juu ya hatari zozote zinazoweza kujitokeza katika biashara/shughuli yake husika.  

Mchumi wa KiAustrian  Joseph Schumpeter  ameielezea dhana ya ujasiriamali kwa kuegemea mihimili ya UGUNDUZI na UBUNIFU, katika nyanja hizi(yaani kugundua na kubuni):-
-Bidhaa Mpya
-Njia Mpya za uzalishaji/uendeshaji.
-Masoko Mapya
-Mifumo mipya ya Vikundi na Mashirikisho

UTAJIRI unapatikana pindi UGUNDUZI unapoenda sambamba na MAHITAJI, kwa mtazamo huu tunaweza kusema ya kwamba kazi ya Mjasiriamali ni sawa na kuunganisha mbegu za vigezo fulani katika hali ya Ugunduzi na Ubunifu ili kutengeneza ubora na thamani kwa mteja kwa imani ya kwamba thamani itakayopatikana itafidia gharama za mbegu hizo, na hatimaye kutengeneza faida ya kutosha inayopelekea UTAJIRI.

Mpaka hapa tumeweza kumfahamu huyu Mjasiriamali kwa maana na Mitazamo michache. Je kila Mfanya biashara ndogo ndogo ni Mjasiriamali? Tathmini hili kabla hujasoma Article nyingine!

Shukrani kwa kuwa pamoja.